Bwege ataka Bombardier zipigwe bei ili Kumaliza Tatizo la Maji Nchini

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara maarufu Bwege amependekeza kuuzwa kwa ndege mbili za Serikali aina ya Bombardier ili fedha zitakazopatikana zitumike kumaliza changamoto za upatikanaji wa maji nchini, kwa madai kuwa zimedumu kwa miaka 57.
Bwege ametoa kauli hiyo leo Mei 8, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19.
Huku akizungumza kwa sauti ya kupanda na kushuka, Bwege amemuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kusimamia upigaji kura wa wabunge, ili kubaini idadi ya wanaounga mkono ununuzi wa ndege hizo na wale wanaotaka fedha kwa ajili ya kuwekeza katika miradi ya maji.
“Leo nakuona kama Spika kweli kweli, upo strong (imara) hongera sana,” amesema na kuwataka wabunge kutoshusha lawama kwa waziri wa wizara hiyo, mhandisi Isaack Kamwelwe na Katibu Mkuu wa wizara, Profesa Kitila Mkumbo kwa madai kuwa bila fedha, hawawezi kufanya lolote.
“Serikali inatakiwa kutoa fedha za maendeleo maana mnachokisema si mnachokitenda. Leo mwananchi umuulize ndege na maji nini kizuri, nyinyi wabunge kama kweli tuwaulizeni kununua ndege na kuwapa watu maji bora nini?”
Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge amesema, “wanaosema inunuliwe ndege na wanaosema tuanze maji wasimame, mkirudi mwaka 2020 (baada ya uchaguzi mkuu) mimi sio Bwege. Mheshimiwa Spika uulize, wanaosema ndege na maji halafu tukawaonyeshe huko, mheshimiwa Spika utaruhusu kweli?  Wabunge tuwaheshimu  mawaziri, sisemi Magufuli mzigo, nasema Serikali ya CCM mzigo.”
Amesema katika jimbo lake amekuwa akiomba mara kwa mara hospitali ya wilaya ipelekewe maji, kwamba akihoji maji anajibiwa ndege kwanza.
“Miaka 57 ya CCM tunaongelea maji? Serikali ya CCM amkeni kama hakuna maji, kama hatupati maji Serikali ya CCM bai bai, maji ni uhai na masheikh wako magereza hakuna maji.”
Amesema kutokana na uhaba huo wa maji ni vyema zikauzwa ndege mbili ili kutatua tatizo la maji, “mheshimiwa Spika kwa kuwa uko vizuri, piga kura anayetaka ndege au maji.”
Mara baada ya kumaliza kuchangia, Spika Ndugai amesema, “hata tukiwalaumu Waziri na Katibu Mkuu tunawaonea. Tukiacha mfuko wa maji, Serikali imetoa asilimia 11, lakini kesho waziri wa fedha, akisimama hapa watueleze. Hivi kama wewe ungekuwa waziri ukisimama hapa utasema nini.”

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *