Mtoto wa Winnie Mandela awaita wanafiki wanaomsifu mama yake baada ya kufa

Mtoto wa Winnie Mandela, Zenani Mandela, ametoa ‘dongo’ mbele ya waombolezaji wakati wa mazishi ya mama yake leo, katika Uwanja wa Orlando, Afrika Kusini.

Zenani amesema, mama yake aliporwa haki yake wakati wa maisha yake.

Leo maelfu ya watu wamekusanyika katika uwanja huo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho mbele ya mwanamapinduzi huyo wa Afrika Kusini, ambaye pia aliwahi kuwa mke wa Nelson Mandela.

Zenani alivicharukia vyombo vya habari na kusema kuwa vilitumika kumchafua mama yake.

“Kwa nini waliukalia ukweli na kusubiri hadi mama yangu afe ndiyo wauseme. Wamepora urithi wa haki wa mama yangu wakati wa uhai wake,” amesema Zenani huku dada yake Zindzi akiwa pembeni yake.

Alionyesha kukasirishwa na kauli ya Kamishna wa zamani wa Polisi nchini humo, George Fivaz, ambaye wiki iliyopita baada tu ya kifo cha Winnie, amesema, hakuna kinachomuhusisha Madikizela Mandela na kifo cha Stompie Seipei.

Inadaiwa kuwa Winnie alihusika na kifo cha Stompie Seipei kijana wa miaka 14, mwaka 1989.

Zenani amesema, wale wote waliomfanyia mabaya mama yake, wasifikiri hata mara moja familia itayasahau mabaya hayo.

“Kumsifia sasa hivi, kunaonyesha wazi jinsi ulivyo mnafiki,” amesema Zenani akimtaja Fivaz.

Ameongeza: “Maumivu aliyoyapata maishani mwake, yapo kwetu.”

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *