Masheikh misikitini sasa kuchaguliwa na BAKWATA.

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limefanya mageuzi makubwa katika kujiendesha kwa kufumua mifumo mbalimbali iliyokuwepo na kuanzisha taratibu mpya ikiwa ni pamoja na upatikaji wa mashehe na maimamu wa misikiti watakaoteuliwa na chombo maalumu badala ya utaratibu uliokuwepo wa kuchaguliwa.

Akitangaza mageuzi hayo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Aprili 5, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, Shehe Khamis Mataka amesema kuwa mageuzi hayo yamefikiwa katika mkutano mkuu uliofanyika Dodoma kuanzia Machi 31 hadi Aprili Mosi.

Shehe Mataka ambaye pia ni msemaji wa Mufti amesema mkutano huo ulifanya marekebisho ya katiba ya Bakwata kwa kufuta mfumo wa uchaguzi wa mashehe wa mikoa, wilaya, kata na maimamu wa misikiti kwa njia ya kuchaguliwa.

Amesema kuwa sasa viongozi hao watakuwa wanateuliwa na vyombo vya kitaaluma ambavyo ni Baraza la Maulama Bakwata Taifa ambalo litakalowateua mashehe wa mikoa na wilaya.

Ameongeza kuwa mashehe wa kata watateuliwa na mabaraza ya mashehe wa mikoa huku maimamu wa misikiti wakiteuliwa na baraza la mashehe wa wilaya.

Shehe Mataka amesema wajumbe hao wapya wa baraza la wadhamini watahakiki mali zote za Bakwata, kuziwekea wakfu ili kuzilinda na aina yoyote ya ufisadi na kwamba, kwenye katiba wameweka kipengele kinachozuia kuuzwa kwa mali ya wakfu kwa namna yoyote ile.

“Changamoto za kimfumo huwezi kuziondoa ila kwa majawabu ya kimfumo. Kwa hiyo changamoto za ubadhirifu na ufisadi uliokuwa unafanywa katika mali za wakfu za Waislamu tumeona jibu lake ni kuwa na kipengele cha kikatiba kinachozuia kuuzwa,” amesema Shehe Mataka.

Kuhusu mapato, amesema kuwa ndani ya Bakwata kulikuwa na ‘pakacha’ lililokuwa linasababisha kupotea kwa mapato na kwa sasa kutakuwa na mfumo mmoja wa ukusanyaji mapato tangu ngazi ya Taifa hadi kata na mfumo wa ukaguzi wa ndani ili kudhibiti mapato hayo.

“Ili kuutekeleza huo mfumo, Bakwata itaweka wahasibu katika mikoa yote na wilaya zote 196 za Bakwata. Kutokana na hali ya baraza ndio kwanza linajijenga, tunatoa wito kwa Waislamu wenye taaluma za uhasibu wajitokeze kuja kujitolea,” amesema.

Hata hivyo, ingawa amesema kuwa Uislamu utajengwa na wenye moyo wa kujitolea, watakaojitolea siyo kwamba hawatapata chochote cha kujikimu na kwamba wakiweza kusimamia vizuri na hali ya kiuchumi ikaimarika wataweza kupata ajira za kudumu.

Kwa upande wake, Mufti Aboubakary Zubeir amesema kuwa yaliyopita yamepita na hawana nia ya kufukua makaburi, bali haja yao ni kuanza safari mpya kuijenga Bakwata.

“Ninachotaka kuwaambia Waislamu na Watanzania kwa ujumla ni kwamba Bakwata sasa hivi inalenga masuala ya maendeleo ya uchumi na elimu katika muondoko mpya,” amesema Mufti Zubeir na kuongeza:

“Pia tunawaomba Waislamu wategemee heri na kwamba Baraza sasa liko katika mfumo kamili na wanisaidie, waache sasa maneno hayatasaidia chochote kama ambavyo wamesema sana wala hakuna msaada katika waliyosema.”Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *