Siku kama ya leo katika historia duniani tarehe 12 March.

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake.

Miaka 164 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkataba wa kihistoria wa Constantinople (Istanbul) ulitiwa saini baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala wa kifalme wa Othmaniyyah. Baada ya nchi hizo tatu kutia saini mkataba huo dhidi ya sera za kujitanua za Urusi ya zamani huko Ulaya, zilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata ushindi dhidi ya Urusi katika vita vya Crimea.

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja.

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *