Bavicha watoa neno kujiuzulu kigogo wake

Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limezungumzia kujiuzulu kwa Naibu Katibu Mkuu wake, Gertrude Ndibalema huku likimtakia kila la heri.

Naibu Katibu mkuu huyo aliyeshika wadhifa huo tangu mwaka 2014 ametangaza kujiuzulu akisema atabaki kuwa mwanachama ili kutimiza majukumu yake binafsi.
Akizungumza leo Machi 12, 2018, Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita amesema hajapata taarifa rasmi ya kujiuzulu huko zaidi ya kusoma kupitia vyombo vya habari.

Amesema iwapo kama kinachoonekana mitandaoni na kuelezwa kuwa ni taarifa kwa umma ni kweli wanamtakia kila la heri huko aendako.

“Ninachofahamu Ndibalema ni mwandishi wa habari na alianzisha programu ya kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali. Nafikiri ameona nafasi ya uongozi aliyopo katika chama ni ya juu huku programu aliyoianzisha inahusisha kuzungumza na viongozi kutoka pande nyingine, ameona haitakuwa sawa,” amesema Mwita.

Mwita alimtaka Ndibalema kufuata kanuni za Baraza kwa kuandika barua rasmi ya kufanya hivyo ili kuruhusu taratibu nyingine ziweze kuendelea.

Gertrude ni kiongozi wa pili wa ngazi ya juu Bavicha kujizulu akitanguliwa na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza hilo, Patrobas Katambi aliyejiunga na CCM.

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *