Mama Diamond ajiondoa kwenye mgogoro wa Zari na Mobeto

DAR ES SALAAM: Mama mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim (pichani) amejitoa kwenye mgogoro unaoendelea kati ya ‘wakweze’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Hamisa Mobeto.

Kabla ya kauli ya mama Diamond juu ya warembo hao mapema wiki hii, wikiendi iliyopita kuliibuka ubuyu kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram kuwa, ugomvi kati ya Zari na Mobeto ulikuwa umeibuka upya baada ya kupoa kwa siku kadhaa.

Uchunguzi ulibaini kwamba, ugomvi baina ya wawili hao ulirejea upya baada ya Mobeto kukutana na Diamond kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika Kitengo cha Ustawi wa Jamii na kukubaliana juu ya malezi ya mtoto wao, Abdulatif Nasibu ‘Prince Dully’.

Ilisemekana kwamba, kuna maneno aliyoweka Zari kwenye Mtandao wa Snapchat yakiashiria kutokuwepo kwa maelewano kati yake na Diamond kufuatia tukio hilo lililoonekana kumweka jamaa huyo karibu na Mobeto.

Kama hiyo haitoshi, kuna ubuyu kuwa, ugomvi huo uliingia hadi kwenye familia ya Diamond ukimhusisha mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’ na mdogo wake aitwaye, Esma Khan ‘Esma Platnumz’.

Kufuatia hali hiyo,alitafutwa mama Diamond na kumuuliza juu ya sakata hilo na kwamba je, ni kweli alikuwa na ugomvi na Zari ambapo aliamua kutoa ya moyoni akisema kuwa, mambo yanayowahusu watu hao hataki ahusishwe nayo.

“Naomba mambo yanayowahusu hao (Zari, Mobeto na Diamond) waulizwe wenyewe mimi simo,” alisema mama Diamond.

Kwa upande wake Esma alisema kuwa, kwa sasa hajishughulishi na mambo ya nyumbani kwao badala yake anadili na maisha ya familia yake na mumewe, Petit Man.

“Kwa sasa siwezi kudili na mambo ya nyumbani kwetu, nadili na maisha yangu na familia yangu,” alisema Esma.

Kwa upande wake, Mobeto, simu yake ya mkononi haikuwa hewani kila ilipopigwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukupokelewa.

Kumekuwa na habari nyingi juu ya kuwepo kwa kutoelewana kati ya Zari na familia ya Diamond huku Mobeto na Wema Sepetu wakihusishwa.

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *