Yaliyotokea siku kama ya leo katika historia duniani tarehe 24 Disemba.

Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu zaidi, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi. Japokuwa kundi hilo la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limefanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao. Kundi hilo linaua hata wazungu wanaotetea haki za makundi mengine. Pamoja na hayo hakujafanyika juhudi kubwa nchini Marekani kwa ajili ya kung’oa kabisa mizizi ya kundi hilo la kibaguzi na lenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Katika siku kama ya leo miaka 493 iliyopita, aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498, baharia huyo wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India.

Miaka 168 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliivamia ardhi ya Guinea huko magharibi mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa nchi hiyo tajiri kwa madini ya dhahabu kudhibitiwa na Ufaransa. Kampuni ya Dhahabu ya Pwani iliundwa huko Guinea kabla ya uvamizi huo ili kuandaa mazingira ya kuingia kimabavu Ufaransa nchini humo.

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi akateuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951.

 

Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *