Mwanamke aliyeuawa na FFU kwa kupigwa risasi kuzikwa kesho.

Mwanamke aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mjini Babati mkoani Manyara, alipokwenda kudai fedha za matumizi ya mtoto anazikwa kesho.

Regina Daniel (29) alipigwa risasi Ijumaa Oktoba 27,2017 na askari Cosmas James aliyekuwa analinda Benki ya NMB tawi la Babati iliyoko Mtaa wa Usalama katika Kata ya Bagara saa 12:30 jioni.

Baba mzazi wa Regina, Daniel Labai akizungumza leo Jumapili Oktoba 29,2017 amesema wanatarajia kumzika kesho Jumatatu Oktoba 30,2017 katika Kijiji cha Mamire wilayani Babati.

Labai amesema hawana chochote cha kusema juu ya tukio hilo zaidi ya kumuachia Mungu.

Amesema wanaiachia Serikali kushughulikia suala hilo kwa kuwa mtoto wao ameshauawa.

“Tunatarajia kumzika Regina kesho Jumatatu na baada ya mazishi na kumaliza msiba ndipo tutajua nini kinachoendelea kwenye suala hilo,” amesema Labai.

Amesema suala la kesi wanaiachia Jamhuri kwa kuwa ndiyo itakayoisimamia itakapoanza mahakamani na wao watabaki kuwa wasikilizaji.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu amesema polisi wanaendelea kumshikilia askari huyo.

Amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa.Author: admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *