Huu ni ushauri alioutoa mwanahabari Luqman maloto kwa meneja Sallam wa diamond kuhusu Ali Kiba
imewekwa na Kibonde
muda 2017-01-10 03:10:52
Watazamaji 139
Huu ni ushauri alioutoa mwanahabari Luqman maloto kwa meneja Sallam wa diamond kuhusu Ali Kiba
Uko hapa : Home > Habari za mastaa>
Inapaswa kufahamika kuwa mkate wa Diamond Platnumz siyo wa Ali Kiba, vivyo hivyo anachostahili Ali Kiba hakiwezi kuwa cha Diamond. Hayo ni madaraja mawili tofauti.
Anayempenda Ali Kiba ana sababu zake alizovutiwa, kama ambavyo walio na mahaba na Diamond wanacho kinachowapendeza. Ni kwa sababu hizohizo wengine wanawapenda wote. Ni kama mimi, nawapenda wote.Nampenda Ali Kiba kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuimba. Sauti yake inakuonesha kuwa hapati shida kufanya anachokifanya, kwamba muziki upo ndani yake. Namfurahia jinsi ambavyo sasa hivi anajituma kufungua milango na madirisha ambayo pengine alitakiwa awe ameifungua miaka mingi kabla.
Nampenda Diamond kwa sababu anavyofanya kazi unaona kuwa anafahamu kuwa muziki ni fedha. Diamond ana kasi nzuri ya utafutaji na kila siku anaonekana ni mwenye njaa ya kufanikiwa. Diamond ametengeneza mzani mzuri kati ya muziki na biashara, na anatoboa.
 
Nampenda Ali Kiba kwa sababu uwezo wake wa kuimba umekuwa kioo cha vijana wengi wanaochipukia, wanatamani kuimba muziki mzuri kama Kiba. Anashirikiana na wasanii wenzake wakubwa na wadogo katika nyimbo zao ndiyo maana anasikika sana. Hivi sasa ameukuza muziki wake na unapaa kimataifa.
 
Nampenda Diamond kwa sababu ndani ya muda mfupi sokoni ameweza kujitengeneza kuwa taasisi imara ya kimuziki. Wasafi Classic Baby (WCB) ni lebo kubwa. Diamond ni bonge la nembo ambayo inatengeneza ajira nyingi. Unawezaje kuacha kumpenda mtu ambaye anapanua wigo wa ajira kwa vijana?
 
NAZUNGUMZA NA SALLAM
Nakubali uwezo wa Sallam ambaye ni meneja wa kimataifa wa Diamond. Jinsi alivyofanikisha colabo kati ya Davido na Diamond katika wimbo Number One Remix, kisha wimbo huo ukafungua njia nyingi za Diamond kimataifa, unawezaje kuacha kumsifu?
Tambo za mafanikio hasa kimataifa ambazo Diamond anapiga, hutakiwi kuacha kumsifu Sallam kwamba anafanya kazi nzuri sana. Diamond amepanuka sana hivi sasa, kwa hiyo haiwezekani kazi zote hizo akawa anafanya peke yake. Wapo wenye kumjenga, Sallam ni miongoni mwao.
 
Hata hivyo, ipo shida moja ambayo Sallam yupo nayo. Hiyo anahitaji kushauriwa. Ni jinsi ambavyo amekuwa akijihusisha na wasanii wenye uhasimu na Diamond. Ni hapo ndipo umeneja wake unapokosa weledi.Wasanii wanaweza kutofautiana na wakawa hawaivi kutokana na sababu za wivu au kuchonganishwa. Msanii anapojiona yeye ni mkubwa, huwa hapendi mwingine asemwe anamzidi au analingana naye. Hapo wivu huibuka kisha chuki hufuata.Mashabiki ndiyo huwagawa zaidi wasanii. Watatokea watu wa pande mbili, hawa watasema huyu zaidi, wale wataibuka na kujibu yule zaidi. Mara zinaibuka timu, mara Team Diamond, ile Team Kiba.
 
Mameneja wazuri hutakiwa kuiona hiyo katika sura ya kibiashara. Inawezekana hata kuibua ‘drama’ za hapa na pale ili kuongeza chachu za kibiashara kwa kila mmoja. Halafu mameneja wenyewe wakihojiwa wanasema ni amani tupu, hakuna chuki, ni hisia tu za mashabiki.
 
Meneja mwingine wa Diamond, Babu Tale, yeye hujua jinsi ya kujibu anapoulizwa kuhusu Kiba na Diamond. Siku zote husema hakuna chuki, kwamba yeye na meneja wa Kiba, Seven Mosha huwasiliana hata kumuomba ushauri.
Kuna siku Babu Tale alisema: “Sisi tuna picha kabisa Ali Kiba na Diamond wakiwa pamoja, tulikutana studio wakapiga, wakazungumza vizuri kabisa, tukitaka kuzitoa tutazitoa. Kwa hiyo maneno ya bifu ni ya mashabiki tu.”
MAKOSA YA SALLAM
Kuna ‘ishu’ ya malalamiko ya Ali Kiba kuzimiwa mic kwenye shoo ya Mombasa Kenya, iliyofanyika kwenye viwanja vya Mombasa Golf Club, lipo pia sakata la Ommy Dimpoz.
Kwanza kabisa, sikubali kuwa Sallam alimzimia mic Ali Kiba. Waandaaji wangeweza vipi kukubali kuhujumiwa onesho lao kubwa namna ile ambalo liliwahusisha wasanii wakubwa duniani, Chris Brown, Wizkid, Vanessa Mdee na Kiba mwenyewe?
 
Huwezi kusema Sallam alikorofisha mitambo akiwa backstage. Mitambo ya muziki haikai backstage. Ingekuwa ni tukio la aina yake sound ya muziki iwekwe backstage.
Hata hivyo, Sallam anajifahamu yeye ni meneja wa Diamond ambaye jamii inafahamu kuwa msanii wake ana uhasama wa kibiashara na Ali Kiba.
 
Onesho lile lilikuwa halimhusu kabisa Diamond, yeye Sallam alikwenda backstage kufanya nini? Backstage ni kwa ajili ya wasanii na timu zao pamoja na waandaaji. Yeye hakuwa sehemu ya msanii yeyote aliyefanya onesho wala uandaaji, kilichompeleka backstage ni nini?
 
Backstage ni eneo maalum la faragha kwa wasanii kujifanyia maandalizi madogomadogo ya mwishoni, kubadili mavazi, kupumzika kabla ya kupanda jukwaani na baada ya kumaliza onesho, au katikati ya shoo msanii anaweza kwenda backstage kubadili nguo, muonekano au kupumzika kidogo kulingana na mpangilio wa onesho lake.
 
Sasa Sallam backstage alikwenda kufanya nini wakati anajifahamu yeye si mhusika? Hivyo basi, ni kweli Sallam hakuzima mic lakini uwepo wake backstage ulitia shaka. Angeweza kukaa maeneo mengine bila kwenda backstage na kwenye stage, yote aliyolaumiwa asingelaumiwa.
 
Tukio la Kiba kuzimiwa mic, linaweza kumfanya Kiba awaze vitu vingi, ikiwemo hilo la kwa nini Sallam alikwenda backstage. Sallam anatakiwa kuacha kujiweka mbele. Maeneo ambayo anafahamu akionekana kimbelembele yanaweza kumuingiza kwenye lawama, anapaswa kujiweka pembeni.
 
Alisema yeye ni meneja na alikuwa kwenye mipango yake ya kutengeneza ‘michongo’, hilo pia ni kosa. Msanii anapoingia ukumbini kazi yake ni kufanya onesho na siyo mambo mengine. Kama ni michongo alitakiwa awafuate mameneja wa Chris Brown na Wizkid hotelini ndipo mazungumzo ya kibiashara yangefanyika, siyo ukumbini,
hasa siyo backstage.
Kingine ni maneno yake baada ya shoo. Yeye kama meneja hakutakiwa kuwa mtu wa kutamka kuwa Ali Kiba anamchukia sana Diamond. Badala yake alipaswa ajitetee kuwa hakuhusika na uzimwaji mic ya Ali Kiba. Ingetosha na angeeleweka, siyo kusambaza chuki.
Maneno yake kuwa Ali Kiba alikataa kupanda jukwaani kabla ya Wizkid akijisema ni msanii mkubwa kuliko Wizkid, hivyo kuwa sababu ya kuharibika kwa shoo ni kumchonganisha Ali Kiba na mashabiki. Kwanza yeye aliyazungumza kama nani? Waandaaji wanasema ulitokea mvurugiko wa ratiba.
 
Kwamba Ali Kiba alifanya shoo yake kwa live-band, Wizkid aliimba playback. Ali Kiba alitakiwa kuimba kabla ya Wizkid lakini ufungaji mitambo ya Kiba ulipochelewa ndipo waandaji waliomba Wizkid aanze kuimba kwanza kuokoa muda. Sallam anapaswa kuchunga maneno yake.
 
Lipo suala la mgogoro wa Diamond na Ommy Dimpoz. Sallam pia akaonekana katikati. Huo siyo umeneja mzuri. Meneja hatakiwi kuonekana akichochea ugomvi kati ya msanii wake na mwingine. Hatari yake ni mbaya sana.
Meneja anatakiwa kuzituliza hisia na hasira za msanii wake pale anapokuwa kwenye migogoro na wenzake. Na ikiwa ndani kwa ndani anaupampu mgogoro uwepo, basi hatakiwi kujionesha. Siyo sasa jinsi Sallam anavyoipampu migogoro ya Diamond na wasanii wengine.
 
HII DUNIA NI DUARA
Sallam amewahi kujiuliza kufanya maisha ya umeneja baada ya Diamond? Nafahamu anamsimamia pia AY, lakini kazi yake namba moja ni Diamond. Je, siku wakigombana itakuwaje?
 
Amewahi kujiuliza kama yeye ni meneja mzuri hata akiachana na Diamond anaweza kuwa meneja wa Ali Kiba au Ommy Dimpoz? Atafanyaje nao kazi ikiwa tayari anatengeneza chuki?
 
Mwenzake Babu Tale ni mjanja ndiyo maana hajiweki mbele, maana anafahamu yapo maisha baada ya Diamond. Sallam anachokifanya ni kama hafikirii kuwa yapo maisha mengine baada ya Diamond.
 
Dunia ni duara, zilishakuwepo nyakati lilikuwepo bifu kati ya Diamond na Rich Mavoko na leo wanafanya kazi pamoja. Ni kama ambavyo Diamond alimpigania Ommy Dimpoz kufika alipo lakini katikati wakagombana.
 
Unapokuwa meneja wa msanii na unapomuona anagombana na wasanii wenzake, kabla ya kujitoa na kuwakabili kwa chuki wale mahasimu wa msanii wako, anza kwanza kujituliza na ujiulize; maisha yako ni yapi baada ya kuachana na msanii wako?
 
Hivyo basi, Sallam hakumzimia mic Ali Kiba, lakini haikufaa kuwepo backstage kwenye shoo ya Kiba ambaye inaaminika na wengi kuwa ana uhasama na msanii wake (Diamond), vilevile hakutakiwa kuzungumza aliyozungumza kuchochea chuki kati ya Kiba na Diamond.
 
Hakutakiwa kuisema shoo ya Kiba kuwa haikuwa nzuri. Hilo ni jukumu la mashabiki na wachambuzi wengine. Yeye anaye msanii waka ambaye inaaminika haivi na Ali Kiba, kwa hiyo maoni yake hayawezi kutenda haki.
 
Ajiangalie pia eneo la Ommy kwa nini aingie katikati na kuonekana anachonganisha mambo? Ommy analalamika kuwa Sallam alimfuata kuomba wamalize tofauti na Diamond, kisha akaenda kusema Ommy ndiye aliyebembeleza kuomba msamaha.
 
Muhimu kufahamu kwa kila mmoja ni hili; ukiwa mwajiriwa usiyejitambua, unaweza kugombana na kila adui wa bosi wako. Ila ukiwa unajitambua utajiuliza kuhusu maisha yako baada ya kuachana na bosi wako. Mwisho utatumia akili yako ya kuzaliwa.
 

Unasemaje kuhusu hii?

babuu ashok alisema, tarehe 2016-01-22 08:15:47:
i like it

Tafadhali coment hapa

Name:
Email:
Message:
 
 
Loading...
Bookmark and Share
deSiGned by sundo